Translate this blog in your favourable language

Saturday, January 11, 2014

ZIFAHAMU TARATIBU NA RATIBA ZA UCHANJAJI WA KUKU KUANZIA VIFARANGA NA KUKU WAKUBWA.

Mtaalam wa Mifugo akiwapa chanjo vifaranga.

Mfugaji akiwapa chanjo kuku

Kuku wakienyeji ni rahisi sana kuwafuga tofauti na wakisasa.

Chanjo kama hii mfugaji unaweza kuchanja kwa maelekezo ya wataalam.

Zipo namna nyingi za uchanjaji wa kuku zingine zinahitaji utaalam

TARATIBU NA RATIBA ZA UCHANJAJI
    Wakati wa kutayarisha mpango wa kuchanja kuku kwa ajili ya kinga dhidi ya magonjwa, kuna vipengele vikuu sita Ambavyo unatakiwa uvifahamu na kuvizingatia. Vipengele hivyo ni kama ifuatavyo:

1. Vifaranga vinavyoanguliwa kwa pamoja:
 Iwapo una kundi zaidi ya moja la vifaranga wanaoanguliwa,
Weka utaratibu wa chanjo ambao utapunguza uwezekano wa magonjwa kuenea shambani. Hivyo basi,
Hakikisha vifaranga na kuku wote wanapata chanjo kwa pamoja.
2. Umri wa kuchanja kuku:
Kwa kuku ambao wanatarajiwa kutaga mayai au kuwa kuku wazazi, chanjo
nyingi hutolewa si zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kuku kuanza kutaga. Pia kuna baadhi ya chanjo ambazo haziruhusiwi kwa kuku wadogo. (Angalia Ratiba).
3. Magonjwa muhimu katika eneo husika:
Ni muhimu sana kuelewa magonjwa ya kuku yaliyopo katika eneo lako kabla ya kuandaa programu ya uchanjaji, hasa kwa yale magonjwa ambayo chanjo zenye
Vimelea hai hutumika. Hivyo basi, sio busara kuanza kutumia chanjo za aina hii katika maeneo ambayo
Ugonjwa huo haujawahi kuripotiwa.
4. Hali ya kiafya ya kuku watakaochanjwa:
 Usiwape chanjo kuku ambao wanaonyesha dalili za kuathirika kwa mfumo wa hewa au wanaonyesha kuwa na minyoo au wadudu wengine. Kwa kuku walio na dalili hizi chanjo zinaweza kuleta madhara na zisifanye kazi.
5. Aina ya kuku watakaochanjwa:
Kuku wanaofugwa kwa ajili ya nyama wanahitaji kinga ya muda mfupi, hivyo basi chanjo moja inaweza kutosha kabla ya kufikia umri wa kuuzwa. Lakini kuku wa mayai na kuku wazazi wanahitaji programu ya chanjo ambayo itawakinga na magonjwa kwa kipindi chote wanapokua na kutaga. (Zingatia Ratiba).
6. Historia ya Magonjwa katika shamba:
Kabla ya kuandaa mpango wa chanjo, lazima ufahamu ni
Magonjwa gani yaliyoenea katika shamba.
a) Kama unataka kuingiza kuku wapya kutoka mahali ambako ugonjwa umeshawahi kutokea,
kuku hao wachanjwe wiki 3 kabla ya kuwaingiza shambani
b) Iwapo utatumia chanjo yenye vimelea hai, hakikisha kwamba magonjwa hayo yameshawahi
kutokea katika shamba husika. Usitumie chanjo hizi katika shamba ambalo ugonjwa huo
haujawahi kutokea au kutambuliwa.
c) Wasiliana na mashamba jirani kufahamu iwapo wanatumia chanjo zenye vimelea hai. Toa taarifa
kwa mamlaka za mifugo iwapo unapanga kutumia chanjo hizo katika eneo lako. Pata ushauri wa daktari.

TARATIBU ZA UCHANJAJI
Mambo muhimu ya kuzingatia:                                                                                         
  •Hakikisha unazingatia kwa makini masharti ya mtengenezaji wa chanjo: jinsi ya kuhifadhi, kutayarisha na njia inayotumika kumchanja kuku. Wakati wote zingatia masharti ya mtengenezaji kuhusu uhifadhi wa chanjo ili isipoteze nguvu.                                                                                                   
 • Fuata ushauri wa daktari wa mifugo unapoandaa programu ya chanjo.                                         
  • Watoa chanjo wapatiwe mafunzo ya jinsi ya kutayarisha na kutoa chanjo                                     
   • Chagua aina ya chanjo kulingana na umri na hali ya kiafya ya kuku.                                           
   • Fanya usafi wa mara kwa mara katika mabanda ili kupunguza wingi wa vimelea kwenye mazingira.
 • Tumia maji ambayo hayajawekwa dawa au kemikali kwa ajili ya kuchanganyia chanjo, k.m. maji ya kisima, mvua, n.k. Maji ya kuchanganyia chanjo yawe na ubaridi, yasiwe moto.                                   
 • Changanya chanjo kabla ya kutumia na iwekwe mbali na kuku.                               
     • Pata ushauri wa daktari wa mifugo kabla ya kuchanja kuku wagonjwa au wale ambao hawako katika muonekano mzuri
• Siku ya chanjo, usiwape kuku maji kwa masaa 3 – 4 ili waweze kunywa maji yaliyowekwa chanjo kwa haraka.                                                                                                                           
 • Zoezi la uchanjaji lifanyike haraka ili kupunguza usumbufu kwa kuku.                                                
 • Tenganisha kuku waliochanjwa na wale ambao hawajachanjwa.                                          
         • Baada ya kuchanjwa, kuku wawekwe kwenye banda linalopitisha hewa vizuri                                                   
 • Baada ya kila zoezi la kuchanja, wafanyakazi wabadilishe mavazi, viatu/buti zisafishwe na kuwekwa dawa, na vifaa vilivyotumika viwekwe dawa ya kuua vimelea.                                                             
   • Fuata utaratibu uliowekwa wa kuharibu/kusafisha vifaa vilivyotumika kuchanja                                    
   • Weka kumbukumbu za uchanjaji vizuri
Mambo ambayo hutakiwi kuyafanya unapochanja

• Kumwaga chanjo ovyo na kuchafua mikono au nguo
• Kuchanganya chanjo za aina mbili au zaidi, isipokuwa pale tu mtengenezaji wa chanjo atakavyoagiza
hivyo, au kwa ushauri wa daktari wa mifugo.
• Kutumia chanjo iliyopita muda wake
• Kutumia chanjo iliyobaki ili itumike kwa kazi ya siku nyingine
• Kuchanja kuku ambao wamepatiwa dawa aina ya antibiotiki.
• Kuchanja zaidi ya chanjo moja kwa wakati, iwapo haikuagizwa hivyo.

CHANJO ZINAZO PENDEKEZWA
Aina ya Chanjo
Umri wa Kuchanja Kuku
Muda kati ya kutoa chanjo
Njia inayotumika kuchanja kuku
Lasota – kwa ajili ya Mdondo/Kideri
Kifaranga wa Siku 3
Rudia baada ya siku 21, baada ya hapo kila baada ya miezi 3
Maji safi yasiyowekwa dawa
Chanjo inayohimili joto - I-2 kwa ajili ya Mdondo/Kideri
Kifaranga wa Siku moja
Rudia baada ya kila miezi 4 kwa kuku wa mayai na wazazi
Tone la chanjo kwenye jicho kwa kila kuku
Hipraviar-B1 - kwa ajili ya
Mdondo/Kideri na Ugonjwa wa Mapafu (Infectious Bronchitis)
Kifaranga wa Siku moja
Rudia baada ya siku 21, baada ya hapo kila baada ya miezi 3
Maji safi yasiyowekwa dawa
VIR-114 – kwa ajili ya Gumboro
Siku 10 au 14
Inaweza kurudiwa Siku ya 17 kwa
wale waliochanjwa wakiwa na Siku
10; na Siku ya 28 kwa wale waliochanjwa wakiwa na Siku 14
Maji safi yasiyowekwa dawa.
Avipro – kwa ajili ya Ndui ya Kuku
Wiki 7 hadi 14
Chanjo moja
Chanja katikati ya ngozi
kwa kutumia utando wa ngozi kwenye bawa
Chanjo ya Mareksi
Kifaranga wa Siku moja
Chanjo moja
Chanja ndani ya tumbo au chini ya ngozi

   Mawasiliano ya Mtaalam 0753226538 kwa msaada zaidi.

YAJUE MAGONJWA MUHIMU YA KUKU/NDEGE WAFUGWAO ILI KUIKINGA NA KUIOKOA MIFUGO YAKO. [KUKU].

Mara nyingi sana kuku mgojwa huwa namna hii,,Ugonjwa ni nini? Ugonjwa ni mabadiliko kutoka katika afya ya kawaida ya mnyama/kuku. Hali hii hutokea pale
vimelea au vijidudu vinapoingia mwili wa mnyama, kwa kula vyakula vyenye sumu, au inapotokea kuna uhaba wa lishe au madini mwilini.
 
TOFAUTI ZA MUONEKANO KATI YA KUKU MWENYE AFYA NA KUKU MGONJWA

KUKU MWENYE AFYA NZURI
Ø  Macho na sura angavu
Ø  Hupenda kula na kunywa maji
Ø  Pua zilizo safi, upanga na undu mwekundu, manyoya
laini na yaliyopangika vizuri
Ø  Hupumua kwa utulivu
Ø  Sehemu ya kutolea haja huwa kavu
Ø  Kinyesi kikavu, cheupe na kisicho na rangi
Ø  Hutaga mayai kawaida

KUKU ASIYE NA AFYA NZURI
Ø  Huonekana mchovu na dhaifu
Ø  Hula na kunywa kidogo au zaidi ya kawaida
Ø  Hutoa kamasi puani, ute na matongotongo; manyoya
yaliyovurugika
Ø  Hupumua kwa shida na kwa sauti
Ø  Sehemu ya kutolea haja inakuwa na unyevunyevu na
kinyesi kuganda
Ø  Huharisha, kinyesi huwa na damu au minyoo
Ø  Hutaga mayai machache au husimama kutaga kabisa
Ø  Huwa na tabia ya kujitenga na wenzake katika kundi
MGONJWA MUHIMU YANAYOSABABISHWA NA BACTERIA
HOMA KALI YA MATUMBO (FOWL TYPHOID)

Maelezo: Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bacteria na hushambulia zaidi kuku
Wakubwa pia na vifaranga. Ugonjwa pia hushambulia aina zote za bata, kanga na ndege
wa porini.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea: Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa
na kinyesi cha kuku wagonjwa. Panya, ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza
ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku waliokufa kwa ugonjwa na kuchafua maji na vyakula.
Maambukizi pia yanaweza kupitia katika mayai yanayototolewa na vifaranga kuathirika. Pia mashine za kutotolea zilizochafuliwa zinaweza kuambukiza vifaranga.

Dalili
Kuku wakubwa
Ø  Kuharisha kinyesi cha majimaji na cha rangi ya njano
Ø  Vifo vya ghafla
Ø  Kupauka kwa upanga na masikio kwa sababu ya kupungukiwa damu
Ø  Manyoya hutimka, hushusha mbawa, hufumba macho na kuzubaa (kuvaa koti)

Vifaranga
Ø  Vifaranga wanatotolewa wakiwa wamekufa au dhaifu
Ø  Hujikusanya pamoja na kukosa hamu ya kula
Ø  Kinyesi cha rangi ya njano na huganda kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja
Ø  Hupumua kwa haraka na kwa shida
Ø  Vifo vingi huweza kutokea kuku wasipotibiwa

Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Kinyesi cha rangi ya njano na kijani kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja kubwa
Ø  Misuli iliyovia na damu kuwa nyeusi
Ø  Ini lililovimba na kuwa na rangi ya pinki
Ø  Bandama lililovimba
Ø  Figo na mayai yaliyovia
Ø  Mabaka meupe kwenye sehemu ya juu ya figo

Tiba
v  Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki ambayo yanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa.
Lakini madawa haya hayawezi kumaliza kabisa ugonjwa kutoka shambani.
v  Pata ushauri wa daktari.

Kuzuia na Kinga
Ø  Hakikisha kwamba vifaranga wako wanatoka katika mashamba ambayo hayana huu ugonjwa
Ø  Panga utaratibu wa kuchunguza afya za kuku wako mara kwa mara na kuondoa/kuchinja kuku
wanaonyesha dalili za ugonjwa.
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi
shambani.
Ø  Fanya usafi wa mabanda na mazingira mara kwa mara unapobadilisha makundi ya kuku kwa kutumia
viuatilifu vilivyopendekezwa.
Aina nyingine ya Homa ya Matumbo (Avian Paratyphoid) inafanana na aina iliyoelezwa hapo juu, tofauti kubwa
ni aina ya vimelea vinavyosababisha aina hii ya homa, na huathiri zaidi kuku na bata wadogo.

HOMA YA MATUMBO (AVIAN PARATYPHOID)

Maelezo: Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bakteria wa spishi tofauti na ya bakteria wanaosababisha homa
kali ya matumbo na hushambulia zaidi kuku na bata wadogo. Vimelea vya ugonjwa huu huweza kusababisha homa ya matumbo kwenye binadamu.


Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Panya, mbwa,
Ø  ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku waliokufa kwa
Ø  ugonjwa na kuchafua vyanzo vya maji na vyakula.
Ø  Maambukizi pia yanaweza kupitia katika mayai yanayototolewa na vifaranga kuathirika. Pia mashine za kutotolea zilizochafuliwa zinaweza kuambukiza vifaranga.

Dalili
Vifaranga
Ø  Vifaranga wanatotolewa wakiwa wamekufa au mara tu baada ya kuanguliwa
Ø  Hujikusanya pamoja karibu na joto
Ø  Uharo kuganda kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja
Ø  Vifo kwenye vifaranga vinaweza kufikia hadi asilimia 50.

Kuku wakubwa
Ø  Vifo vya ghafla Kuharisha kinyesi cha majimaji na cha rangi ya njano
Ø  Kuku kuharisha
Ø  Kupungua kwa uzito
Ø  Kuku wa mayai hupunguza utagaji
Ø  Kuku anaonekana mchovu

Uchunguzi wa Mzoga
Mabadiliko muhimu katika mzoga wa kifaranga ni:
Ø  Ini kuvimba na kuvia
Ø  Uvimbe mweupe mdogo mdogo kwenye ini
Ø  Mapafu kuvia
Ø  Utumbo kuvimba
Ø  Njano ya yai kutapakaa tumboni

Tiba
Ø  Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki na sulfa ambayo yanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na
ugonjwa. Lakini madawa haya hayawezi kumaliza kabisa ugonjwa kutoka shambani.
Ø  Pata ushauri wa daktari.

Kuzuia na Kinga
Ø  Hakikisha kwamba vifaranga wako wanatoka katika mashamba ambayo hayana huu ugonjwa.
Ø  Panga utaratibu wa kuchunguza afya za kuku wako mara kwa mara na kuondoa/kuchinja kuku
wanaonyesha dalili za ugonjwa.
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi
shambani.
Ø  Fanya usafi wa mabanda na mazingira mara kwa mara unapobadilisha makundi ya kuku kwa kutumia
viuatilifu vilivyopendekezwa.
Ø  Mayai yakusanywe mara kwa mara
Ø  Hakikisha vifaranga wanapata joto la kutosha.

KUHARISHA KINYESI CHEUPE (BACILLARY WHITE DIARRHEA)
Maelezo
Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bakteria na hushambulia zaidi kuku wadogo wenye umri hadi wiki tatu. Ugonjwa pia hushambulia aina zote za bata, kanga na ndege wa porini (mbuni).

Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Panya, ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku iliyokufa kwa ugonjwa na kuchafua maji na vyakula.
Ø  Kuku waliopona baada ya matibabu wanaweza kuendelea kuchafua mazingira na kuwa chanzo cha
maambukizi, hivyo waondolewe shambani.
Ø  Maambukizi pia yanaweza kupitia katika mayai yanayototolewa na vifaranga kuathirika.
Tahadhari: Wageni na wafanyakazi wanaweza kusambaza ugonjwa kutoka shamba hadi shamba au
banda hadi banda.
Ø  Vituo vya kutotolea vifaranga vinaweza kuwa chanzo. Hakikisha vifaranga wako hawatoki kwenye kituo chenye kuku wagonjwa.

Dalili
Vifaranga
Ø  Vifo vya ghafla
Ø  Vifaranga wanatotolewa wakiwa wamekufa au dhaifu
Ø  Hujikusanya pamoja karibu na taa kwa ajili ya kupata joto
Ø  Uharo wa rangi nyeupe kama chaki
Ø  Hupumua kwa shida
Ø  Uharo huganda kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja
Ø  Vifaranga wanapiga sana kelele
Ø  Vifaranga wanaonyesha ulemavu
Ø  Kuvimba magoti

Kuku wakubwa
Ø  Kuku wakubwa huonyesha dalili za ugonjwa sugu
Ø  Kupauka kwa upanga na masikio kwa sababu ya kupungukiwa damu
Ø  Utagaji wa mayai hupungua

Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Njano ya yai iliyotapakaa tumboni mwa kuku
Ø  Uvimbe mdogo mdogo wa rangi ya kijivu ulioenea kwenye moyo,firigisi, misuli, mapafu na sehemu ya nje ya utumbo katika kuku wakubwa (umri wa wiki 2 hadi 5)

Tiba
Ø  Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki ambayo yanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa.
Ø  Lakini madawa haya hayawezi kumaliza ugonjwa shambani kabisa.
Ø  Pata ushauri wa daktari.

Kuzuia na Kinga
Ø  Hakikisha kwamba vifaranga wako wanatoka katika vyanzo vilivyothibitishwa kuwa havina huu ugonjwa
Ø  Tengeneza utaratibu wa kufanya usafi wa mabanda na mazingira mara kwa mara unapobadilisha makundi
ya kuku kwa kutumia viuatilifu vilivyopendekezwa.
Ø  Panga utaratibu wa kuchunguza afya za kuku wote wenye umri zaidi ya miezi mitano (5) mpaka hapo
kundi lote litakapoonyesha kwamba hakuna kuku mwenye maambukizi, kuku salama wahamishiwe
katika mabanda safi.
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi
shambani au bandani.

KIPINDUPINDU CHA KUKU (FOWL CHOLERA)
MAELEZO
   Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bacteria ambao huenea kwa haraka na kusababisha vifo vingi. Ugonjwa hushambulia kuku na ndege wa aina zote ijapokuwa jamii ya bata huathirika zaidi kuliko kuku.

Google+ Badge