Translate this blog in your favourable language

My pager view

Thursday, October 24, 2013

HIVI NDIVYO EDO KUMWEMBE ALIVYOLIA NA WATANZANIA KUKOSA UZALENDO, SAMATA, HASHEEM THABIT WAHUSISHWA AMKUMBUKA MAXIMO.


Soma makala kutoka kwa Edo Kumwembe na ona jinsi alivyogusa mambo muhimu tunayokosa watanzania wengi,, inasikitisha.


Samatta, Hasheem na ujinga wa kutojipenda

NA EDO KUMWEMBE

      NCHI inaliwa usiku na mchana. Unajua kwanini? Achilia mbali tamaa binafsi zilizojaa katika mioyo yetu, lakini asilimia kubwa ya Watanzania hatuitazami nchi yetu katika jicho la uzalendo.
Edo Kumwembe
Huyu anashirikiana na mzungu kuingia mkataba duni wa Madini, yule anashirikiana na mgeni kuingia porini kuua Tembo na kutoweka na meno yao. Matokeo yake barabara nzuri za Lami zinajengwa Ulaya, vijijini kwetu tunaachiwa mashimo.
      Kwetu sisi, mtu akipata kazi TRA tunamwambia ‘Kazi kwako, ushindwe mwenyewe kujenga sasa’. Hii ndio Tanzania kadri niijuavyo. Mtu hana habari kwamba huyo mtu anayemshawishi kujenga ndiye mwenye mamlaka ya kusimamia kodi zetu.
Uzalendo ni neno gumu kwa Mtanzania. Hata katika michezo ni hivyo hivyo. Mwaka 2006, mgeni mmoja alisafiri kilomita 8945 kutoka Rio de Janiero mpaka Dar es salaam kwa ajili ya kuwafundisha Watanzania jinsi ya kuipenda timu yao ya taifa.
     Ni Marcio Maximo. Mbrazil huyu alisafiri kutoka kwao kuja kutuelekeza jinsi ya kuvaa jezi za Taifa Stars, jinsi ya kuvaa skafu, jinsi ya kushangilia wachezaji wetu uwanjani. Aibu iliyoje! Mpaka leo Watanzania wanakiri hili hadharani. Kwanini tulishindwa kulitambua hili kabla hajafika?
     Wakenya wana matatizo yao. Lakini nje ya matatizo yao, Mkenya akimuona mwenzake, basi anajihisi kama anajitazama mwenyewe. Ni kama ilivyo kwa Waingereza, Wacongo, Wamarekani, Wanigeria na wengineo. 
Wanamuziki wa DR Congo kazi yao kubwa ni kusifia watu wao. Nyakati Fulani nilikuwa nasikiliza nyimbo zao na muda mwingi walipenda kumtaja Dikembe Mutombo. Staa wa zamani wa Kikapu wa NBA aliyezaliwa Kinshasa.
Umewahi kumsikia Mwanamuziki wa Tanzania ameimba wimbo na kumtaja Hasheem Thabeet? Katika ubora wake wa sasa hivi, umewahi kufikiria Diamond Platinum anamtaja Hasheem katika wimbo wake walau mmoja?
Lakini pia umewahi kufikiria katika mahojiano yoyote ambayo Hasheem anaweza kufanya na CNN au kituo chochote cha Televisheni duniani anaweza kusema anavutiwa na nyimbo za Diamond au Juma Nature ambaye alikuwa akimpenda sana wakati yupo shuleni Makongo? Hapana.
     Sehemu ya ndani ya mioyo yetu haitutumi kujipenda. Inatutuma kuwapenda zaidi wengine. Kama Hasheem Thabeet angekuwa Mkenya, Watanzania tungemfuatilia kwa umakini zaidi.
Na ndio maana kwa kufuta ujinga huu, nilianza kwenda Lubumbashi kwanza kueleza jinsi Mbwana Samatta anavyoishi kifahari nchini humo, kabla ya kwenda Italia kueleza jinsi McDonald Mariga anavyoishi. Tanzania kwanza, Afrika Mashariki na dunia baadae!
      Mara kadhaa katika mahojiano yake na vyombo vya habari, Obi Mikel huwa anasema anavutiwa na wanamuziki ndugu wa kundi la P Square. Na wanamuziki hawa wakihojiwa kuhusu wanasoka wanaowapenda huwa wanaanza na Obi Mikel. Wote ni Wanigeria hawa. Kwao, maisha yanaanzia nyumbani!
Carlos Tevez akifunga bao huwa anaonyesha fulana yake ya ndani iliyoandikwa jina la Fuerte Apache. Hiki ndio kitongoji alichotoka pale Buenos Aires, Argentina. Lakini umewahi kufikiria kwamba siku moja Samatta atavua jezi yake na kutuonyesha fulana iliyoandikwa Mbagala, eneo alillokulia?
      Hawezi kufanya hivi. Hajafundishwa uzalendo. Na wakati mwingine unajiuliza, kwanini umlaumu wakati hata nyumbani kwake pale Lubumbashi sebuleni hakuna bendera ya Tanzania? Watu wanaochota pesa Serikalini kwa madai ya kuitangaza Tanzania wamewahi kuwasiliana naye?
Majuzi kulikuwa na picha imeenea katika mitando mbalimbali ya kijamii ikimuonyesha Robin van Persie na Hasheem Thabeet wakiwa wamepiga picha jijini London. Ni Van Persie mwenyewe ndiye aliyekuwa ameituma picha hiyo katika mitandao.
      Cha ajabu, kuna baadhi ya Watanzania walianza kuhisi kwamba picha hiyo ilikuwa imetengenezwa tu kiubunifu na watu wa mitandaoni. Aibu iliyoje! Kuna ajabu gani mwanasoka nyota wa Ligi Kuu ya England akapiga picha na mchezaji kikapu wa NBA. Au kwa sababu mcheza kikapu huyo ni Mtanzania? Kujidharau kulikopitiliza.
Wakati Francis Cheka alipompiga bondia wa Marekani, Phill Williams Agosti mwaka huu, mashabiki wakaanza kukejeli kwamba Cheka alikuwa amempiga Kinyozi tu kutoka Marekani. Ni kweli kwamba Williams anamiliki Saluni nchini Marekani. Lakini si hata Cheka anaokota chupa za maji pale Morogoro? Wote ni mabondia wa kulipwa lakini wana shughuli zao nje ya ulingo wa ngumi.