Translate this blog in your favourable language

My pager view

Wednesday, January 5, 2011

umuhimu wa kula nanasi msimu huu wa mananasi jenga afya.


msimu wa mananasi umeshawadia katika ukanda wote wa pwani. Katika msimu huu bei ya nanasi nalo hushuka na kuwa katika bei ambayo mtu yeyote anaweza kuimudu bila shaka. Hivyo asiyekula mananasi ya kutosha mpaka msimu unaisha, huyo ana hasara kubwa katika afya yake. Ukiacha ukweli huo, tunda hili lina faida ambazo linashawishi kila mtu kulitumia.Faida zinazoweza kupatikana kwenye nanasi ni nyingi ambazo zinaweza kuwa kama kinga na tiba kwa baadhi ya matatizo ya kiafya ambayo pengine yangehitaji mtu kwenda hospitali kupatiwa dawa, tena kwa gharama kubwa. Miongoni mwa faida hizo ni hizi zifuatazo:
KUIMARISHA NURU YA MACHO
Inawezekana karoti ikawa ndiyo inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho, lakini nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho. Utafiti unaonesha kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo mitatu kwa siku, kunaondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36 kwa watu wazima.
KINGA YA MWILI
Nanasi linaaminika kuwa miongoni mwa matunda yenye chanzo kizuri cha vitamin C ambayo kazi yake mwilini ni kuupa mwili kinga dhidi ya ‘wavamizi’ mbalimbali (free radicals), ambao wanapoingia mwilini, kazi yao hua ni kuharibu chembembe hai za mwili. Vile vile ‘wavamizi’ hao wanapoweka makazi mwilini, huziba mishipa ya damu na hivyo kusababisha magonjwa ya moyo na mengine mengi, ikiwomo kansa ya tumbo.
Kwa kuongezea, vitamini C inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuifanya kuwa kinga ya magonjwa madogo madogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi mengine. Unapokuwa na kiwango cha kutosha cha vitamin hiyo, bila shaka kinga yako ya mwili itakuwa imeimarika na hivyo utakuwa umejiepusha na maambukizi mbalimbali.
USAGAJI WA CHAKULA
Nanasi lina virutubisho vinavyouwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo, pindi mfumo huu unapowezeshwa kufanyakazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa wakati kama inavyotakiwa. Hivyo wenye kula tunda hili kwa wingi hawawezi kusumbuliwa na taizo la ukosefu wa choo. Aidha, kwa mujibu wa tafiti nyingine, nanasi pia lina virutubisho vyenye uwezo wa kupunguza au kuzuia uvimbe tumboni.
Mara baada ya nanasi kumenywa na kukatwa vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu kwa ajili ya kuliwa baadaye, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo chenye mfuniko (container) ili kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi hadi cha siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha. 
ILA ZINGATIA HILI
unapokula tunda lolote, zingatia usafi. Osha tunda hadi litakate, nawa mikono yako kwa sabuni au maji moto, kisha shika tunda lako, vinginevyo unaweza kujikuta unakula tunda na vijidudu vya maradhi ya kuharisha na hata kipindupindu.nk 
mwisho wa makala fupi ya nanasi na steven mruma